Katika Maisha yetu ya kila siku mara nyingi tunajikuta katika mazingira yanayotulazimu kufanya maamuzi magumu au kuchagua kitu katikati ya vitu vingi ambavyo vinatuchanganya akili. Wengi wetu kwa ugumu huu wamejikuta wakifanya maamuzi mabovu na kuchagua chaguzi mbovu ambazo ama ziliwapa hasara au ziliharibu kabisa muelekeo au mustakabali wa maisha yao. Ndio maana wenzetu wa magharibi (Ulaya) wanamsemo usemao “Life is how you make decisions” Maisha ni vile unavyofanya maamuzi.
Tunavyofanya maamuzi fulani, hususani katika kuchagua vitu kati ya vingi hatumaanishi vyote au vile vingine ni vibaya bali hatuwezi kuvichagua vyote kwa wakati mmoja na hivyo tunalazimika kufanya maamuzi ya kuanza na kimoja na kumalizia na vingine.
Mfano: Msichana aliyeomba kazi na wakati huo huo ameomba nafasi ya chuo na pia yuko katika mahusiano na mchumba wake anayehitaji waowane. Hali hii inamfanya msichana huyu kuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi nini afanye kwanza na nini kifuate badae.
Daima huwezi kufanya vitu vyote vilivyo mbele yako, huwezi kuchukua kila fursa inayokujia lazima uwe na uwezo wa kufanya maamuzi yaliyo bora. Maamuzi haya yatachangia sana katika kufika mwisho wenye ushindi au katika kufikia mwisho wenye majuto na machozi.
Katika makala hii nitajaribu kukupa mbinu tofautitofauti ambazo zitakuwezesha kufanya maamuzi yako kwa haraka, kwa ubora na bado ukawa katika uwezo wa kuyasimamia maamuzi hayo.
1. Angalia na zitafute fursa mbalimbali
- Jambo la kwanza ni uwezo wa kuzidaka fursa pale zinapojitokeza
- Jambo la pili ni uwezo wa kuzitengeneza fursa wewe mwenyewe
Katika jambo la kwanza, la uwezo wa kuzidaka fursa, namaanisha kuwa, baada ya kueleza au kutangaza kwa marafiki na kupitia njia mbalimbali kuwa unataka au kutafuta kitu au kazi fulani, haupaswi kukaa tu kimya na kulala, fursa zaweza kwanza kuja kupitia marafiki zako, wafanyakazi wenzako, au kupitia matangazo uliyoyafanya maeneo mbalimbali, sasa hapa haustahili kulala bali kuzidaka na kuzifanyia kazi fursa hizo.
Katika jambo la pili, namaanisha uwezo wa kuzitengeneza fursa wewe mwenyewe. Kama kweli unahitaji kitu lazima ufungue macho kutafuta nini tatizo la jamii inayokuzunguka, wakati wote tatizo au hitaji la jamii laweza kugeuzwa kuwa fursa. Mfano, kama sehemu ni kame na maji ni tatizo jitahidi kuchimba kisima, kwa kutatua tatizo lililosumbua jamii umepata fursa ya kufanya biashara. Usikae tu na kusubiri fursa zijihudhurishe miguuni pako zenyewe. “run for them”.
Njia zote hizi mbili hazinabudi kutiliwa mkazo na kila mtu.
a) Jizindue wewe mwenyewe
Mara nyingi tunasikia neno uzinduzi. Hapa naamanisha tendo la kuchukua na kuuendea mkondo uliouchagua ukutoe kimaisha. Anza kupiga mbio kwenye njia unayoona itakutoa. (fanya uzinduzi wako mwenyewe bila kusubiri ufanyiwe). Ili kuweza kujizindua pasipo kuchelewa, lazima kufuata ushauri ufuatao.
· Jiulize Swali “Ni nini?”.
Kila wakati jiulize ni nini ninachotaka kukifanya na katika hiki ninachotaka kukifanya, ni nini ninachotaka kukipata?
Unaporuhusu akili yako kufahamu ni nini unachotaka kukipata, unauruhusu mwili na nafsi yako kujitia nguvu tayari kwa kukiendea hicho kitu.
Faida nyingine ya kujiuliza ni nini ninachokitaka ni kukupa picha ya ukubwa au umuhimu wa kile unachokitaka ili uweze kuandaa kila kinachowezekana kama vile rasilimali vitu au rasilimali watu, au rasilimali fedha ili kuhakikisha unakipata kile unachokihitaji.
· Uwe tayari kupata hasara! (be a risk taker) Kama wewe ni mwoga wa kushindwa au mwoga wa kupata hasara kamwe hutoweza kujizindua kwa haraka. Kwa ajili hii lazima ujue jinsi ya kushuhulikia hizo hofu zako. Usiogope kupata hasara katika chochote ufanyacho maana kupitia hasara tunajifunza mbinu bora zaidi za kuitafuta faida kubwa.
b) Yatumie vema na kwa ufanisi maamuzi yako.
Ili uweze kuyatumia vema na kwa ufanisi maamuzi yako, tu utumie mfano huu. Jifikirie umebeba glasi tupu mkononi mwako, waweza kuijaza glasi hiyo kwa majuto na lawama za uliyowahi kuyafanya au waweza kuijaza kwa yale uliyojifunza huko nyuma kwaajili ya kesho yako. Kama utabaki kujuta na kulaumu yaliyopita au uliko sasa hutofaidika chochote kiujuzi kwa ajili ya kesho yako. Lakini kama utafanya kila unalokutana nalo kuwa ni somo utapata ujuzi tele kwa kesho yako.
Pinga tabia ya kulaumu na kujutia maamuzi yako kwa kuzingatia ukweli kwamba
· Mambo mengi hutokea au hutegemea na mitazamo uliyonayo.
Maamuzi mengi tufanyayo hutegemea na mitazamo tuliyonayo maishani. Kama mtazamo wako ni wakujutia kila kitu au kulaumu wengine, basi utalaumu na kujutia kila utakachowahi kukifanya, mfano; utajutia na kulaumu kozi unayosoma, kazi unayofanya, biashara unayofanya, mke au mume mliyeoana nae, watoto uliowazaa nk.
· Maamuzi ufanyayo yanategemeana sana na mfumo wako wa maisha. maamuzi yako maishani hutegemea sana na kile unachokiamini. Kile ulichotayari kukisimamia na kukitetea, hutegemea sana uasili wa maadili yako, kupitia hivi vitu tunapata maamuzi mabaya au maamuzi mazuri. Mfano; maamuzi ya mtu mwenye maaadili ya kidini ni tofauti na maamuzi ya yule asiye na dini.
ITAENDELEA ALHAMIS IJAYO USIKOSE KUIFUATILIA HAPA HAPA www.chrismauki.com

0 comments:
Post a Comment